kipa yanga akamatwa



WAKATI Yanga ikijiandaa na mchezo muhimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, kipa namba tatu wa timu hiyo, Said Mohamed, juzi alishikiliwa kwa muda na Jeshi la Polisi, baada ya kumshambulia askari wa kike wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Tukio hilo lilitokea eneo la Kivukoni wakati basi la timu hiyo lililokuwa limewabeba wachezaji likiwa mbioni kuvuka kuingia Kigamboni ambako timu hiyo ilikwenda kufanya mazoezi.
Chanzo cha habari kinaeleza kuwa wakati basi hilo likijiandaa kuvuka ng’ambo, mmoja wa maaskari wa kike katika kivuko hicho, Mariam Rashid, aliingia ndani ya basi walilokuwemo wachezaji hao kwa lengo la kukagua tiketi zao, ndipo wachezaji hao walipoanza kumshambulia kwa maneno.
Mohamed, kipa wa zamani wa Majimaji ya Songea, alianza kumshambulia askari huyo kwa matusi ya nguoni na baadaye kumtemea mate usoni, mara baada ya tukio hilo, kipa huyo alishikiliwa na askari waliokuwepo eneo hilo na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Kivukoni kisha kuhamishiwa Kituo cha Kati na kushikiliwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa huru kwa dhamana.
“Unajua lilikuwa ni tukio la kushangaza sana, watu wengi hawakulitarajia lakini tunashukuru Mungu alipofikishwa kituoni akaweza kuwekewa dhamana na kiongozi wa timu, alitakiwa kuripoti kituoni kesho (jana),” kilisema chanzo hicho.
Championi Ijumaa lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Faustine Shilogile, ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kesi hiyo yenye RB namba CD/RB/3169/2012, bado inafanyiwa uchunguzi na Jeshi la Polisi.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment

Designed by Mustapha E.Hanya +255 732 575 718.