MBIO za Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zimezidi kuwa ngumu baada ya jana kukutana na kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Toto African, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.
Yanga ambayo ilikuwa chini ya kocha wake mkuu, Kosta Papic, ambaye alizomewa na mashabiki mara baada ya mechi hiyo, ilipata wakati mgumu kukabiliana na wenyeji wao hao ambao walioonyesha dhahiri kuwa na nia ya kuibuka na ushindi baada ya kucheza kwa kujituma hasa kipindi cha kwanza.
Mshambuliaji Musa Said ndiye aliyekuwa chachu ya kupeleka majonzi kwa Yanga baada ya kufunga mabao mawili katika dakika ya 18 na 40 huku Iddy Moody akifunga moja katika dakika ya 24.
Hamis Kiiza, raia wa Uganda ambaye amekuwa akicheka na nyavu katika mechi za hivi karibuni, aliifungia Yanga mabao yote mawili katika dakika ya 43 na 65, huku shuti kali alilopiga kipindi cha kwanza likigonga mwamba na kurejea uwanjani.
Kutokana na kasi ya mchezo, mpaka dakika 90 zinakamilika, Yanga ilikuwa imepata kona sita huku Toto ikiambulia moja.
Mara baada ya mchezo huo, makocha wa Yanga hawakutaka kuzungumza na waandishi na wakati wakitoka uwanjani hapo, mashabiki kadhaa waliusubiri msafara wao na kuwazomea, lakini zaidi ilikuwa ni kwa Papic ambaye alikuwa amepanda kwenye gari aina ya Noah.
Aidha, mwamuzi wa mchezo huo, Judith Gamba, alimtoa nje kocha wa Toto, Athuman Bilal, kutokana na kuingilia maamuzi kadhaa ya mchezo huo, mara baada ya kutolewa nje, Bilal aliangusha chozi huku akilalamika kisha akaelekea jukwaa kuu.
Kutokana na matokeo hayo, Yanga imesalia katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43, Toto imefikisha pointi 23 ikiwa katika nafasi ya 10, Simba ndiyo kinara ikiwa na pointi 53, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 50.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment