SIMBA YAENDA ALGERIA KIJESHI

SIMBA inaondoka keshokutwa Jumatatu kuelekea Algeria huku kocha wake, Milovan Cirkovic, akijigamba ameandaa mbinu za kijeshi kwa ajili ya kuing'oa Entente Setif ya huko kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Milovan anakipeleka kikosi chake baada ya kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza. Simba inahitaji ushindi, sare au kufungwa chini ya mabao mawili ili iweze kusonga mbele, timu hizo zitarudiana Ijumaa ijayo huko Setif, Algeria.

Mserbia huyo ametoa tamko hilo zito akielewa kuwa wana kibarua cha kukabiliana na fitina za Entente Setif ndani na nje ya uwanja huko Algeria.

Milovan alikiri kuwa kikosi chake kinatakiwa kucheza kwa nguvu mchezo huo na ndiyo maana ameandaa mbinu za mithili ya za kijeshi ili kuhakikisha wanaibuka kidedea.

Mambo ya fitina za Waalgeria yamethibitishwa na kiongozi wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma Algeria, Issa Matimbwa, alipozungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu jana Ijumaa.

Simba itaondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri na italala jijini Cairo, Misri na siku inayofuata itakwenda Algeria.

Mazoezi ya Milovan
Cirkovic alisema amewaandaa wachezaji wake kuwa fiti kama wanajeshi ili washambulie kwa kasi katika dakika za mwanzo na kupata bao la kuwamaliza nguvu Entente waliowahi kuwa mabingwa wa Afrika mwaka 1988.

Mserbia huyo alisema pia amewaandaa vijana wake kumiliki mpira kwa muda mwingi ili kuwapa wakati mgumu Waalgeria hao.

"Unajua mbinu nzuri ya kujihami siyo tu kukaa nyuma, bali pia kumiliki mpira," alisema.

Milovan alisema katika maandalizi ya timu yake, aliweka mkazo wa kumaliza tatizo la washambuliaji kukosa mabao ambalo lilijitokeza katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Washambuliaji wa Simba katika mchezo huo walikosa nafasi nyingi za wazi, Emmanuel Okwi pekee alikosa nafasi tano wakati Felix Sunzu alipoteza mbili.

�Kitu kikubwa ambacho tunatakiwa kukifanya ni kumaliza kazi mapema ndani ya dakika 45 za kwanza, halafu tuimarishe ulinzi ili wasipate goli na hilo linawezekana," alisema.

�Najua watakuwa kwao na wanaweza kutumia mbinu mbalimbali na hata chafu, lakini tutapambana nao."

Mazoezi ya penalti
Kocha huyo alikazania sana suala la kumiliki mpira kwa wachezaji wake ili waweze kulimudu pambano hilo kwa kiasi kikubwa kwani timu nyingi za Waarabu huwa zina sifa ya kumiliki mpira.

Pia kocha huyo alikuwa akiwapa wachezaji wake mazoezi ya upigaji wa penalti kila siku katika kambi hiyo ili kama ikifika hatua hiyo basi wachezaji wake wasipatwe na hofu.

Simba inaweza ikafika hatua ya penalti endapo itafungwa ugenini mabao 2-0 na ndiyo maana kocha huyo amekuwa akilikazania suala la upigaji penalti.

�Ingawa penalti huwa wanasema hazina ufundi, lakini ni muhimu kuwapa mazoezi wachezaji kwani hii ni soka na lolote linaweza kutokea hivyo inatakiwa tujiandae kwa hali yoyote ile,� alisisitiza.

Kupuliziwa dawa ya usingizi
Simba itakuwa na kazi mbili kubwa kukabiliana nazo katika mchezo wao dhidi ya Entente Setif kwani watatakiwa kukabili fitina za Waarabu na hali ya hewa ya baridi kali.

Entente Setif inaongozwa na tajiri Abdelhakim Serrar ambaye ni mwanasoka wa zamani anayefahamu fitna za soka, ambayo ni hulka ya timu za Kiarabu.

Matimbwa alisema kuwa Simba wasijidanganye wakadhani wamemaliza kazi kwa ushindi wa nyumbani wa mabao 2-0.

"Kwa hawa jamaa ngoma bado ni mbichi, hawana tofauti na timu nyingine za Afrika Kaskazini," alisema Matimbwa anayesoma Shahada ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Algeria.

Matimbwa alitadharisha kuwa Simba watapaswa kuweka watu wa kulinda vyumba vyao vya kubadilishia nguo muda mwingi wa mchezo kwani Waalgeria wana kawaida ya kupuliza dawa za usingizi (nusu kaputi) wakati wa mapumziko ya mechi.

Alitolea mfano yeye (Matimbwa) alifanya kazi hiyo wakati Taifa Stars ilipocheza na Algeria huko Blida, Algeria mwaka juzi na timu hizo zikafungana 1-1.
"Nililinda vyumba vya Stars lakini bado walinivamia na kutaka kunipiga, niliwagomea kabisa wasifanye mbinu zao chafu," aliongeza Matimbwa.

Alisema mbinu ya kupulizia dawa vyumbani ndiyo mara nyingi hutumiwa na timu za Afrika Kaskazini kuzimaliza timu zinazotoka kusini mwa Jangwa la Sahara.

Matimbwa alionya pia kuna uwezekano mkubwa kwa uongozi wa Entente kuingiza mashabiki wake bure ili kuwapa hamasa wachezaji wao.

Alisema mashabiki hao wanashangilia timu zao kwa unazi mkubwa kwa hiyo Simba wanapaswa kulifahamu hilo.

Pia alionya kuwa mashabiki wa Algeria wana vurugu akitaja timu zilizowahi kufanyiwa vurugu kama Rwanda, Misri na klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Baridi kali hadi barafu kudondoka
Matimbwa alitahadharisha kuwa Simba wanapaswa kujiandaa kukabiliana na baridi iliyoko Setif, ambako hufikia barafu kudondoka.

Alieleza kuwa Setif ni tofauti na sehemu nyingine za Algeria kutokana na sehemu hiyo kuwa na mwinuko.

Matimbwa anaeleza kuwa baridi ya Setif ni kali na humalizika mwezi Mei ikiwa tofauti na sehemu nyingine za Algeria ambako humalizika mapema.

Alisema mji huo uko kwenye mwinuko mkali wa mita 1,100 kutoka usawa wa bahari kufanya hali yake ya hewa kuwa nzito sawa na miji kama Johannesburg (Afrika Kusini) na Addis Ababa (Ethiopia).

Matimbwa alitahadharisha hali hiyo inaweza kusababisha mtu akashindwa kupumua vizuri na hata kutoka damu puani.

Simba imejipanga
MWENYEKITI wa Kamati ya Ufundi, Ibrahim Masoud �Maestro� aliiambia Mwanaspoti wanafahamu changamoto walizonazo na wamejipanga kukabiliana nazo.

Maestro alisema Simba siyo wageni wa fitina za Waarabu kwani walikumbana na mengi walipokutana na Wydad Casablanca ya Morocco jijini Cairo, Misri.
Alisema pia kuwa wamejiandaa vizuri kukabiliana na hali ya hewa ya huko wakifahamu fika kuwa hivi sasa kuna baridi kali.

"Tunajua pia kutakuwa na fitna chafu kabla na hata wakati wa mchezo, tumejipanga kuziba mianya yote ya fitna hizo," alisema.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment

Designed by Mustapha E.Hanya +255 732 575 718.