FUNGA MDOMO KAULI YA SIR

LONDON, ENGLAND
HALI si shwari kwa vigogo wa jiji la Manchester, ushindani wa ubingwa unaendelea na vita ya maneno imekolea.

Baada ya chokochoko za kiongozi wa Maendeleo ya Michezo wa Manchester City, Patrick Vieira, kocha wa Manchester United Alex Ferguson amesema kuwa amechoshwa na matamshi ya mchezaji huyo wa zamani wa Man City na kuwa kinachofuata ni kufunguliwa mashtaka katika Chama cha Soka England (FA).

Ferguson alirusha maneno makali zaidi baada ya kusema kuwa wachezaji wake ni watu wa mbio ndefu za marathoni, si mbio fupi kama walivyo Manchester City.

Kauli za kocha huyo zimekuja baada ya kukasirishwa na maneno ya Vieira, ambaye juzi Alhamisi alitamka hadharani kwamba kikosi cha Manchester United kinapendelewa na marefa.

Lakini Ferguson alisema kuwa Vieira, ambaye kwa sasa ni mmoja wa viongozi wa Manchester City, anastahili kushtakiwa kwa kutamka maneno makali kwa waamuzi ambao hufuata kanuni.

Ugomvi kati ya Ferguson na Vieira ulianza wakati Vieira alipomponda kocha Ferguson kwa kumwambia kuwa alikuwa na kiwewe ndiyo maana alimrudisha Paul Scholes katika kikosi licha ya kwamba nyota huyo alishastaafu.

Lakini Ferguson alisema kuwa Man City wamechanganyikiwa ndiyo maana wamemrudisha Carlos Tevez licha ya kwamba mchezaji huyo alionyesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu.

Wakati malumbano hayo yanaendea, mbio za ubingwa nazo zinapamba moto, leo Jumamosi Manchester City wana nafasi ya kuongeza presha kwa wapinzani wao Manchester United kama wataishinda Sunderland.

Hata hivyo, timu hiyo itakaa kileleni kwa muda mfupi tu kwani kama Manchester United ikishinda dhidi ya Blackburn keshokutwa Jumatatu itarudi katika nafasi ya kwanza.

Kikosi cha Roberto Mancini kilikalia kiti cha uongozi kwa saa chache Jumapili iliyopita baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Stoke City lakini Manchester United iliwazidi kwa pointi tatu baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Fulham.

Ingawa Manchester United inaonekana kama vile itakutana na vibonde, Blackburn iliwahi kushinda katika Uwanja wa Old Trafford msimu huu, ilikuwa Desemba mwaka jana ambapo walitoka kifua mbele kwa mabao 3-2.

Huku zikiwa zimebaki mechi nane tu kabla ya kumalizika msimu na timu mbili za jiji la Manchester zikiwa na matarajio ya kukutana Aprili 30, kila timu haitaki kupoteza mchezo.

Nayo Chelsea inaendelea vizuri na wiki hii iliichapa Benfica bao 1-0 katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na inategemewa kuonyesha ukali wakati itakapocheza na Aston Villa leo Jumamosi

Lakini, hata kama watashinda bado hawatakuwa katika nafasi nzuri kwani kikosi cha Roberto Di Matteo kipo nyuma ya Tottenham inayoshika nafasi ya nne kwa pointi tano. Nayo Arsenal inaweza kujishindilia katika nafasi ya tatu kama itaifunga QPR.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment

Designed by Mustapha E.Hanya +255 732 575 718.