simba ya sajili mabeki wawili

PAMOJA na kuwa katika hatua za mwisho kumsajili beki kisiki wa APR, Mbuyu Twite, uongozi wa Simba umeanza mazungumzo na beki mwingine ngangari, Gladys Bokese.
Twite au Bokese, mmoja wao ataziba pengo la Kelvin Yondani ambaye ametua Yanga na beki Lino Musombo aliyesajiliwa kutoka DC Motema Pembe ya DR Congo ameonekana kushindwa kukidhi mahitaji ya Simba.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinaeleza, uongozi wa klabu hiyo umefanya mazungumzo na Twite ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ pamoja na Bokese aliyewahi kung’ara katika klabu ya DC Motema Pembe pamoja na Etoil du Sahel ya Tunisia.
“Wote tumefanya nao mazungumzo, inaonekana ni wachezaji ambao wanalingana viwango. Kitu kizuri kuhusiana nao ni kwamba, wana kasi, nguvu na ni wazuri kwa mipira ya juu.
“Tatizo lililoonekana ni uchezaji wa Musombo na Nyosso kuwa wa aina moja, hivyo tunahitaji mtu wa aina ya Bokese na Mbuyu,” kilieleza chanzo.
Kuhusiana na hilo, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, alikiri kufanya mazungumzo na mabeki hao wawili.
“Kweli tumezungumza na Mbuyu na Bokese, lakini kuna mambo ya kumalizia. Yeyote kati yao atajiunga na Simba kabla dirisha la usajili halijafungwa,” alisema Kaburu.
Tatizo kubwa kwa Twite ambaye ni chaguo la Simba lilikuwa ni kuhusiana na pacha wa Mbuyu aitwaye Kabange Twite.
“Wote walitaka kuja pamoja lakini ingekuwa vigumu kwa Simba kwa kuwa sasa haihitaji kiungo wa ukabaji kwa kuwa tuna Mussa Mudde. Mwisho, Mbuyu ameelewa na amekubali kuja Simba,” kilieleza chanzo.
Mbuyu na Kabange wamekuwa wakihama pamoja kutoka timu moja kwenda nyingine, walitokea FC Lupopo ya DR Congo, wakajiunga na APR na baadaye kuchukua uraia wa Rwanda. Mwaka juzi, Mbuyu aligoma kwenda Ubelgiji baada ya klabu moja ya nchi hiyo kumtaka yeye tu na mdogo wake abaki Rwanda.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment

Designed by Mustapha E.Hanya +255 732 575 718.