KOCHA WA SIMBA AMUITA NGASSA SIMBA SC

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, ameziponda propaganda za baadhi ya viongozi wa Azam FC kulalama kuhusiana na mshambuliaji wao, Mrisho Ngassa na kusisitiza kuwa anamhitaji.
Milovan, raia wa Serbia, amesema anamhitaji Ngassa katika kikosi chake na amewasilisha ombi kwa uongozi wa Simba na ikiwezekana litakuwa ni jambo zuri kwake.
“Nimewaambia viongozi tumpate Ngassa kama kuna uwezekano. Ni mmoja wa wachezaji bora na atakuwa na msaada kwetu,” alisema Milovan.
Simba imeanza kulishughulikia suala la kumnasa kiungo huyo ingawa suala la Azam FC kuona inaweza kupata nafasi ya pili na kushiriki michuano ya kimataifa linaweza kuwa kikwazo.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alikataa kuweka wazi kuhusiana na suala hilo na kusema bado ni mapema sana.
Lakini mmoja wa viongozi wa chini kabisa wa Azam FC, Jaffari Idd, alionekana kutojua lolote na kuanza kulalama kwenye vyombo vya habari, eti kuandikwa kwa habari ya Ngassa ni sawa na kuihujumu timu hiyo!
Iwapo Simba itampata Ngassa aliyeng’ara akiwa na Yanga kabla ya kutua Azam FC kwa kitita cha Sh milioni 98, maana yake itakuwa imeongeza nguvu kubwa ya mashambulizi.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment

Designed by Mustapha E.Hanya +255 732 575 718.